01.10.08 - ICTR/GOVERNMENT II - MAHAKAMA YA ICTR KUTEMBELEA MAENEO YALIKOFANYIKA MAUAJI YA RWANDA

Arusha, 01 Oktoba, 2008 (FH) - Mahakama namba II ya Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR) inayosikiliza kesi ya maauji ya kimbari dhidi ya mawaziri wanne wa zamani wa Rwanda, Jumatatu ijayo itaanza ziara ya wiki moja kutembelea maeneo ambayo watuhumiwa hao wanasadikiwa kutenda makosa hayo mwaka 1994.

0 min 46Approximate reading time

Watuhumiwa katika kesi hiyo ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Afya, Casimir Bizimungu, waziri wa zamani wa Biashara, Justin Mugenzi, aliyekuwa waziri wa Utumishi wa Umma, Prosper Mugiraneza na waziri wa zamani wa Mambo ya Nje, Jerome Bicamumpaka.

Kwa mujibu wa ratiba ya ziara hiyo, jopo la majaji watatu litakaloongozwa na Jaji Kiongozi Khalida Khan kutoka Pakistan, waendesha mashtaka wa ICTR na timu za mawakili wa utetezi katika kesi hiyo, wataanza ziara yao kuanzia Oktoba 6, 2008 hadi Oktoba 10, 2008. Majaji wengine katika jopo hilo ni Lee Muthoga wa Kenya na Francis Shorts kutoka Ghana.

Ratiba hiyo pia imeonyesha kwamba katika ziara hiyo watatembelea maeneo mbalimbali yakiwemo 23 yaliyopo katika miji ya Kigali, Kabuga, Kibungo, Gitarama na Gisenyi.

Wakati upande wa utetezi ulihitimisha kesi Juni 12, 2008 kwa kuwasilisha mashahidi wake 114, mwendesha mashtaka alifanya hivyo miaka mitatu iliyopita baada ya kuleta mashahidi wake 57 wa kuunga mkono mashtaka yake dhidi ya watuhumiwa.

Kesi hiyo ilianza kusikilizwa Novemba 2003.

NI

© Hirondelle News Agency